Na Mwl Oscar Samba
Siku Moja Nikiwa katika chuo cha Biblia, Mwalimu wangu aliingia darasani na kututaka kila mmoja wetu kutoa andiko ambalo lipo moyoni mwake ama analolipenda sana. "Mostly favourite verse" nami nilitoa hili hapa; Mathayo 11:6 Naye heri awaye yote asiyechukizwa nami.
Andiko hili nililipata wakati napitia mazingira magumu sana kimaisha, kimahusiano, kihuduma na kadhalika. Nadhani unafahamu kwamba kwenye maisha kuna nyakati zinatukabili ambapo mtu huweza kujikuta ukihoji uwepo wa Mungu maishani mwako, na hata kujihoji wewe mwenyewe kama kweli umeambatana vyema na huyu Mungu!
Sio jambo geni sana, maana hata Yesu aliwahi kupitia hapo, alipokuwa msalabani aliuliza kwa Baba yake mbona amemuacha..? Sasa, nami nikiwa katika hali ya namna hiyo, ndipo Mungu alipozungumza nami kupitia hilo andiko.
Nami sina budi kukutia moyo katika makala hii ya kwamba Mungu anakwambia yu na heri mtu yule asiyechukizwa naye. Mtu ambaye yu tayari kuvumilia lolote kwa ajili yake. Fahamu sana kuwa msisitizo ni heri au baraka zi juu ya yule ambaye hachukizwi na njia ambazo Mungu anampitisha, bila kujali ugumu na uzito wake.
Mazingira ya andiko hili, ama mukutadha wake ni kwamba; Yohana Mbatizaji, ama aliye babaye wa kiroho wa Yesu Kristo, ambaye pia alimtambulisha, sanjari na kumbatiza katika ubatizo wa maji mengi, sanjari na kushukiwa na Roho kwenye ubatizo huo: alikuwa akipitia mahali pagumu sana.
Alikuwa ametupwa gerezani, mbele yake hapana shaka aliona ugumu uliomkabili ikiwemo hatari ya kifo. Baya ama gumu zaidi hata Yesu mwenyewe hakwenda kumtembelea. Hakutuma hata ujumbe wa kumtia moyo.
Yohana yule yule aliyetutambulisha kwa ujasiri mkuu, na kuhusika katika ubatizo wake na ujio ama utambulisho wa Roho wa Bwana juu ya Yesu, alifikia hatua ha kuwa na shaka. Akili yake ilianza kuingiwa na shaka iliyotokana na ugumu ama uzito wa jaribu.
Inawezekana nawe umewahi kuhubiri tena kwa ujasiri mkubwa sana kuhusu huyu Yesu na uweza wake. Umekuwa ukimsema mbele ya kusanyiko na hata kwa mtu mmoja mmoja umekuwa ukimshuhudia hivyo. Na hakika katika hilo wao na wewe mmekuwa mkimuona; akiokoka na kuponya. Shubuda zako na zao pia zipo.
Lakini umekuwa ukipitia mahali pagumu, mahali ambapo hata wewe mwenyewe huelewi ni kwa nini unapitia hapo. Akili zako zimefikia alipofikia Yohana Mbatizaji. Kuna muda unaona kama vile Mungu amekusahau, ama amegoma kukusaidia. Umekuwa ukijaribu kuitafuta dhambi uliyoitenda bila kuiona. Umekuwa ukitubu na kutubu. Hata jamii yako nayo imekuwa ikiona ama ikikuona kama mtu aliyekosea ama mtu ambaye lazima itakuwa kuna dhambi umetenda ndio maana unapitia hapo.
Umejaribu kujitetea kuwa haipo, wala wao hawakuelewi, maana kwao haiwezekani upite hapo. Mwanzo wa jaribu walikuwa pamoja nawe, ila sasa hawakuelewi. Wamegeuka kuwa marafiki wataabishaji kama wale wa Ayubu.
Nafsi yako imechoka kiasi cha kutamani kurudi nyuma, ama hata parapanda ingelia leo. Inafika hatua ya kujiuliza maswali mengi kama haya ya Yohana; Mathayo 11:2 Naye Yohana aliposikia huko gerezani matendo yake Kristo, alituma wanafunzi wake, kumwuliza,
:3 Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?
:4 Yesu akajibu akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohana mnayoyasikia na kuyaona;
:5 vipofu wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema. 6 Naye heri awaye yote asiyechukizwa nami.
Kitu kimoja wapo kinachonishangaza ni hiki! Maneno ya Yesu baada ya Wanafunzi wa Yohana kuondoka. Haya hayakusikika masikioni mwa Yohana maana wajumbe wake walikuwa wameshaenda. Yesu anaelezea jinsi mbingu zinavyomuona Yohana, jinsi alivyo mkuu. Hata heshima ya kipindi cha ukurasa wa Agano Jipya unatajwa kama enzi za Yohana. Lakini kiuhalisia Yohana hajui hili. Ni sawa na Ayubu, mbingu zinamsifia Ayubu, mbingu zinajigamba na kujivunia yeye, lakini yeye yupo mahali pagumu. Tena katika ugumu huo hasikii hata sauti ya hizo sifa.
Ni hatati sana kujiona kama jamii inavyokuona, kuwa ni mtu uliyefilisika, ni mtu uliyeachika kwenye ndoa yako. Ni mtu usiye na kibali, ni mtu wa kutangatanga. Ni mtu uliyekosa heshima. Muhubiri mmoja akahubiri akasema kwamba Daudi alikuwa mpakwa mafuta lakini hapo awali alikataliwa, maana alirudishwa tena machungani. Eliabu kaka yake alimbeza na kumsuta. Akasema kwa lugha ya kingereza, "anoited but rejected."
Haya maisha huwa nayafahamu sana, maana nimeyaishi kwa muda mrefu. Ila ukiwa ni mtu uliyejifunza kujiona kama uliuyo kwa sura ya Kiungu, lazima utamuona au utayaona maneno ya Yesu hata alipokuwa yu mbali na wajumbe wa Yohana. Utayaona maneno ya Mungu kwamba hakuna mkamilifu kama Ayubu, mwenye haki na mwenye kumcha Mungu. Mtu ambaye mbingu zinapendezwa naye.
Ni hatari ukakubali kujiona kama adui zako wanavyokutazama, walimuona Yusucu ni mtu mmbaya wakamtupa shimoni, wakamuuza kwa Waishumali, Waishumali nao hawakuziona akili zake njema wakamuuza kwa Mmisiri. Huko nako mke wa Potifa akamuona kama anayestahili kuutosheza mwili wake. Akaonekana muhalifu mbele za Potifa na kutupwa gerezani. Ila Farao akamuona kwa jicho la Kiungu, ndipo alipoamua kumtoa gerezani. Na kumfanya kuwa Waziri mkuu.
Unapawa kuuona uwaziri mkuu ukiwa kwenye shimo ulilowekwa na ndugu zako. Unapaswa kuuona uwaziri mkuu ukiwa bado ni mfanyakazi wa ndani ama mtumwa kwa Potifa. Unapaswa kuuona uwaziri mkuu ukiwa jela.
Najua ukiwa kwa wazazi ni rahisi sana kuuona uwaziri mkuu, maana katika maono hatua ya awali huwa na imani kubwa sana. Ila inapofika swala la njia hapo ndipo wengi hukwama.
Mtu mmoja aliniambia maneno haya wakati ninapitia pito la mahusiano kuwa; Mungu aliwaambia wana wa Israel kule Misri uzuri wa Kanani ikiwemo Maziwa na Asali, ila hakuwahi kuwaambia changamoto za Jangwani.
Wengi waliyaona maziwa na asali kiwepesi, hawakuona maji machungu ya Mara, hawakuwahi kuyaona maisha kabla ya maji ya Moriba, hawakuwahi kuziona nyoka za moto. Kwenye fikra zao hakuwahi kufikiri kuchoshwa na chakula cha mana kiasi cha kukumbuka matango, matikiti maji na hata vyakula vya viungo vya vitunguu swaumu huko Misri.
Shule ya Mungu hawakuwahi kuijua. Ni watu wachache wenye uwezo wa kuyaona maisha ya Kanani ya Maziwa na Asali katikati ya maji machungu ya Mara, katikati ya kiu kali ile ya Moriba. Ni wachache wenye uwezo wa kutazama juu ya mti na kumuona nyoka wa shaba hapo na kuweka tumaini lao. Wengi hutafuta kutazama jeraha na kusikia maumivu badala ya kutazama mtini. Aliyeangikwa mtini amebeba tumaini. Ukitazama jeraha utapoteza hilo tumaini.
Yote katika yote fahamu sana kuwa Njia za Mwenye Haki sio njia nyepesi. Wala hazikuwahi kuwa hivyo. Tafadhali tazama pamoja nami wasifu huu muhimu wa Yohana ambao hata yeye mwenyewe hakuwahi kuusikia. Ili uweze kuelewa ni kwa jinsi gani mbingu zinakutazama, tofauti kabisa na unavyofikiria au kujifikiria.
Mathayo 11:7 Na hao walipokwenda zao, Yesu alianza kuwaambia makutano habari za Yohana, Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini? Unyasi ukitikiswa na upepo?
:8 Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa mavazi mororo? Tazama, watu wavaao mavazi mororo wamo katika nyumba za wafalme. 9 Lakini kwa nini mlitoka? Ni kuona nabii? Naam, nawaambia, na aliye mkuu zaidi ya nabii.
:10 Huyo ndiye aliyeandikiwa haya, Tazama, mimi namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako mbele yako. 11 Amin, nawaambieni, Hajaondokea mtu katika wazao wa wanawake aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji; walakini aliye mdogo katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko yeye. 12 Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka.
:13 Kwa maana manabii wote na torati walitabiri mpaka wakati wa Yohana.
Itaendelea Wakati Ujao...
http://www.ukombozigospel.blogspot.com
Tumeunda Channel ya WhatApp, Tufolo; https://whatsapp.com/channel/0029Va827LBJENy9u6Enke1h
Kundi letu la WhatsApp https://chat.whatsapp.com/E0eD0xegh1eIGMjRykPyRD
Telegram https://t.me/+fft3GHXC9xIzYjhk
Subscribe YouTube yetu: https://www.youtube.com/@ukombozigospeltv
Kwa Maombi +255759859287
Usiache Kutembelea na Ku-Like Page Yetu Ya Mafundisho ya Neno la Mungu Facebook: https://www.facebook.com/MafundishoyanenolaMungunamwalimuoscarsamba?mibextid=ZbWKwL
Nikutakie Siku Njema
USIKATE TAMAA, YESU YUPO KAZINI.
"Kesho Yako ni Nzuri Kuliko Leo Yako."
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni