Mwalimu Oscar:
Mwl OSCAR SAMBA ( #NasahazaMwlOscar )
#FaidayaJaribu: #Usiogope
Ni Sehemu ya Kitabu Chetu Tarajiwa cha FIKRA SAHIHI KATIKA SHAMBA LA BWANA. Pwenti ya 18.
18. Ni Kiongozi Mwenye Mfumo wa Maisha, na Mfumo wa Uongozi Kama Mtumishi au Mtumikiaji na Sio Mtumikiwa. "Servanthood."
Huyu ni kiongozi ambaye sio bunyenye, kama aliyekuwa mkuu wangu wa chuo Mzee Marehemu Jonas Mkoba alivyopenda kusisitiza.
Huyu ni kiongozi ambaye hatafuti ukuu katika ulimwengu huu wala katika maisha yake ya kiuongozi. Anaishi maisha ya kujinyenyekeza au kujinyenyekesha kama mtoto. Yesu alilijua hili, na alilichukia na kulionya sana. Maana kanuni moja wapo yakuwa mkubwa mbinguni ni kuwa mdogo duniani. Aliwaambia wanafunzi wake ambao waliuliza swali zuri sana tu, ya kuwa ni nani aliye mkubwa mbinguni _ya kwamba huyo aliyemkubwa huko ni yule aliye mdogo huku au humu ulimwenguni.
Anaposema usipoongoka, uwe na hakika ananena habari za usipobadilika. Kuongoka ni kubadilika kwa nia ya kubadilisha fikra au akili zako ama mtazamo; ni katika mfumo au maana ya kutubu. Biblia moja wapo ya kiswahili yenye kutumia kiswahili kile chepesi imetumia maneno kubadilika au kubadilishwa. Linalolandana na Biblia kadhaa za kingereza.
Kwa mantiki hiyo ni dhairi ya kuwa Yesu aliliona hili, na alipoliona akagundua fikra zao zisipobadilika na kufikia au na kuwa kama mtoto mdogo ambaye hatafuti makuu, kuna mahali hawawezi fika; Mathayo 18:1 Saa ile wanafunzi wakamwendea Yesu wakisema, 2 Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao, 3 akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.
4 Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni. 5 Na ye yote atakayempokea mtoto mmoja mfano wa huyu kwa jina langu, anipokea mimi;
Aliyemkubwa mbinguni, au mwenye kuheshimika siye yule mwenye kutafuta heshima hapa duniani. Bali ni yule mwenye kujishusha.
Siku hizi kumeibuka wimbi la wahubiri wenye fikra za ajabu sana, wenye akili ambazo hata Shetani anapigwa na butwa nazo. Kwao ni kusaka tu ufahari, ataongozana na walinzi kama kiongozi wa Ikulu, ataongozana na msafara wa magari ya kifahari, wengine wanatumia paka kapeti jekundu kama Rais anapokuwa akitoka safari!
Ukitaka kuongea naye lazima utangulize maneno kama Mheshimiwa Nabii, Mheshimiwa Mtumishi wa Bwana, na kadhalika. Akiongea unaitikia kwa heshima ndiyo baba!
Ndiposa Yesu akasema mtu asiwaite baba maana baba mnaye mmoja tu mbinguni wala mtu asiwaite mwalimu maana yupo mmoja...
Hakuwa na nia ya kutuzuilia kuitwa hivyo kwa maana ya utambulisho, ila alikuwa na nia ya kutuzuilia kuviweka vyeo hivyo moyoni. Sasa hawa ambao hadi liwekwe jina Mheshimiwa ndipo kuwe na kuonekana kwamba wameheshimiwa, uwe na hakika wamepotea zaidi.
Yule kijana tajiri alipomfuata na kumuita mwema Yesu alikataa! Marko 10:17 Hata alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele? 18 Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu.
Sio kwamba Yesu hakuwa mwema! Alikuwa mwema, ila alikuwa anampa somo la kuepuka kumtukuza kwa staili ya kunuia kuwafundisha wanafunzi wake pamoja na mimi leo kutokukubaliana na utukufu unaolengwa kwenye nafsi zetu za uongozi au vyeo.
Hili ni muhimu sana kulifahamu. Utukufu ukikuingia moyoni ndio mwanzo wa kugombana na Mungu. Ni mwanzo wa kuanza kutoka kwenye kusudi, ni dalili, ni matokeo na pia ni sababisho la kiburi ama kupotea kwa unyenyekevu. Hali inayozaa kuachwa, na kughadhabikiwa na Mungu.
Kiongozi ni mtumishi wa anao waongoza. Ni mtumwa wao, yupo hapo ili kuwatumikia. Sasa wale waliopotoka ndio ambao huhitaji kutumikiwa, hadi kuandaliwa zulia jekundu na kulazimisha heshima. Akija kanisani na hajapokewa mkoba basi siku hiyo ibada nzima itavurugika, maana ni kugombana mwanzo mwisho. Ila Yesu hakuwa hivyo. Ni vyema kuwafundisha kuheshimu viongozi, lakini usilazimishe heshima, na hata ikikosekana tazama ni kwa nini huwa unaumia.
Je, unaumia kwa sababu watoto wako kiroho wanakosa thawabu za kuheshimu wanaowaongoza kama Warumi 13 inavyofundisha au moyo wako unaumia kwa sababu hujapokea utukufu? Kilichompoza Sauli mfalme ni hiki, ya kwamba Daudi wamempa makumi elufu na yeye maelufu tu!
Sasa nini kitakachofuata kama sio ufalme? Wivu ukazaliwa hapo, mwanzo wa kutaka kumua Daudi ukachipuka! Hiyo ni 1 Samweli 18.
Kwa hiyo chanzo kikubwa cha migogoro kati ya watumishi chipukizi ambao karama na kibali kimeonekana kwao humu makanisani au kwenye huduma, na wachungaji au viongozi wao ni hii roho au tabia ya utukufu. Ya kwamba, wivu unaibuka baada ya wao kuanza kupata kibali, ikiwa ni matokeo ya kuhisi utukufu wao umemegwa!
Umewahi kulelewa na mchungaji ambaye ili afurahi au akupende lazima umsifiye! Akikupa kuhudumu usipomsifia hutapata tena nafasi. Ila anayemsifia ndiye mwenye kibali kwake. Kwenye hili eneo nilikuwa makini sana, nilijua adhari zake katika kuharibu moyo wangu, sikuwa tayari kujiharibu ili kumridhisha.
Yesu anatuambia ya kuwa alikuja kutumika, sio kutumikiwa! Kiongozi wa aina hii ni mnyenyekevu. Kwake kuchimba mtaro wa kanisa, au kujihusisha kwenye ujenzi pamoja na washirika wake ni jambo la kawaida kabisa. Hatafuti ukuu, wala makuu.
Siku kadhaa nilikuwa natoka safari naelekea mkoa fulani kuhudumu, nikiwa katika kituo cha magari au mabasi mwenyeji wangu akaja na kunikuta nikiwa nabeba mizigo yangu; alishangaa na kushituka huku akiniambia kuwa sikustahili kubeba mimi! Nilijua fika kuwa mfumo wake ni kwamba wapo vijana wa kumsaidia mtumishi, wao ni watumwa wangu na mimi ni mkuu wao. Ni aibu kwa mtumishi kufanya kazi kama hizo. Ni kama vile zinaondoa upako, heshima na kadhalika. Na ukililea kanisa hivi ni umekosea sana.
Kuna ina kuu mbili ya utukufu, kuna utukufu wa Mungu kwa mtu, na kuna utukufu wa wanadamu kwa mtu. Wengi wakishapoteza utukufu wa Mungu kwa watu; kinachofuata ni kujiwekeza sana kwenye utukufu wa wanadamu kwao.
Paulo alishona mahema na bado upako ulikwepo. Nikienda kwa mshirika nikamkuta anapasua kuni na mimi kumsaidia kubeba hainiondolei upako. Ukishirikiana nao kufanya usafi kanisani haiondoi upako, wala kuondoa heshima, Yesu alikula nao, na aliwanawisha miguu na bado haikuondoa heshima yake kwao.
Sijui kama unajua funzo kuu katika jambo au tukio hili la Yesu...ni kutufundisha utumishi kama sehemu ya kuwatumikia; sisi tuwe watumishi wao. Na sio kuwa watumikiwa; Yohana 13:6 Hivyo yuaja kwa Simoni Petro. Huyo akamwambia, Bwana! Wewe wanitawadha miguu mimi?
7 Yesu akajibu, akamwambia, Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye. 8 Petro akamwambia, Wewe hutanitawadha miguu kamwe. Yesu akamwambia, Kama nisipokutawadha, huna shirika nami.
9 Simoni Petro akamwambia, Bwana, si miguu yangu tu, hata na mikono yangu na kichwa changu pia. 10 Yesu akamwambia, Yeye aliyekwisha kuoga hana haja ila ya kutawadha miguu, bali yu safi mwili wote; nanyi mmekuwa safi, lakini si nyote.
Nimekupatia maandiko yote ili ikitokea ukawa na mwanafunzi kama Petro ujue namna ya kumsaidia. Mfundishe, maana unaweza kujikuta una mshirika aliyelelewa kwenye mifumo fulani ya kunyenyekea watumishi kama anavyopaswa kumnyenyekea Yesu, akajikuta anakuwa na ugumu wa kukubaliana nawe au kukuelewa. Unapaswa kumfundisha.
Hata ukisahau yote hapa! Kumbuka hili; ya kwamba wewe ni mtumwa wao; sio bunyenye ama mtumikiwa.
Mathayo 20:20 Ndipo mama yao wana wa Zebedayo akamwendea pamoja na wanawe, akamsujudia, na kumwomba neno. 21 Akamwambia, Wataka nini? Akamwambia, Agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako. 22 Yesu akajibu akasema, Hamjui mnaloliomba. Je! Mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi? Wakamwambia, Twaweza.
23 Akawaambia, Hakika mtakinywea kikombe changu; lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu. 24 Na wale kumi waliposikia, waliwakasirikia wale ndugu wawili.
25 Lakini Yesu akawaita, akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. 26 Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu;
27 na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; 28 kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.
Kwa hao wana na mama yao tunapata thima ya kuepuka kutaka vyeo, au heshima. Maana nafasi nyingine hupewa waliokwisha kuandaliwa na Baba tayari. Lakini kwa hao 10 ambao waliwakasirikia hawa, tunajifunza somo la kuepuka kuwa na uchu wa nafasi kiasi cha kuwaonea wengine uchungu, wivu na hata hasira. Leo hii swala hili limeshamiri sana hususani kwa viongozi wa makanisa au madhehebu yaliyokua. Kadri dhehebu lako linavyokua, ndivyo jitihada za kusaka nafasi zinavyoongezeka.
Kuna watumishi wamekuwa ni "ant soacial" yaani hawachangamani na wenzao, wala washirika. Kama kuna maisha ya ushirika ninajifunza mahali basi ni kwa Yesu, ninajifunza hili jambo sana. Alikula na kulala na kuishi na wanafunzi wake, wala hakuogopa kuwekewa sumu kama hivi leo ilivyogeuka na kuwa kisingizio kikubwa. (Alikuwa social Being.)
Napenda sana hili jambo kwa Yesu. Aliongea na kila mtu, hakuhitaji barua ya maombi ya kuonana naye; leo hii imekuwa ni vigumu kuonana na watumishi fulani kuliko unavyoweza kueleza; sio kwamba hana muda, ila ni nani anayetaka kumuona! Ndicho kigezo.
Kwa yule anayeweka kipaumbele cha fedha, ili kumuona; huyo ni mlanguzi ni jambazi hafai: wala sio mtumishi wa Mungu ni mganga njaa ni mchumia tumbo kama mzee wangu Joans Mkoba alivyokuwa akitusisitizia: kwa hiyo achana naye.
Tuna watumishi chumia tumbo. Kwao kutumika bila masilahi sio sifa yao; bali sifa kwao ni kuchumia tumbo. Na fedha ndugu zangu hazijaagi.
Narudia tena, ewe mshirika unayefuatilia kitabu hiki, mtumishi kama huyu ni tapeli, kaanaye mbali. Ukiendelea kumuendekeza utafilisika. Maana hawa wanakuwaga na mapepo au maroho, au wengine wanatengenezewa dawa na waganga wa kienyeji ili kuweza kuwavuta watu wawaletee fedha. Ndiposa utamkuta mtu anaambiwa kalete kiasi fulani, naye anapambana hadi anakipata, yupo tayari kuuza kila kitu ili aipate tu hiyo fedha! Sio yeye, bali ameshalogwa akili. Ukitaka kuamini mtake atoe sadaka yake kwenye ujenzi wa kanisa lilo hai; atatoa kila aina ya sababu. Watu hawa wanajiunganisha na madhabahu zenye hizo roho; na kinachofuta ni wao kuwa mateka kwenye akili zao. Ukiweza waombee badala ya kuwacheka na kuwalaumu tu.
Wewe mtumishi unayeanza tabia za utapeli au kupenda fedha mwisho wake ni aibu kubwa sana. Ndio mwanzo wa kujikuta unageukia msaada wa nguvu za kigeni ili upate tu fedha. Unaacha utumishi na kuwa mtumikiwa; bunyenye.
http://www.ukombozigospel.blogspot.com
Tumeunda Channel ya WhatApp, Tufolo; https://whatsapp.com/channel/0029Va827LBJENy9u6Enke1h
Kundi letu la WhatsApp https://chat.whatsapp.com/E0eD0xegh1eIGMjRykPyRD
Telegram https://t.me/+fft3GHXC9xIzYjhk
Subscribe YouTube yetu: https://www.youtube.com/@ukombozigospeltv
Kwa Maombi +255759859287
Usiache Kutembelea na Ku-Like Page Yetu Ya Mafundisho ya Neno la Mungu Facebook: https://www.facebook.com/MafundishoyanenolaMungunamwalimuoscarsamba?mibextid=ZbWKwL
Nikutakie Siku Njema
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni